Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT),
imewalipa zaidi ya Sh4.4 bilioni wakulima wa pareto katika mikoa ya
Mbeya, Njombe, Iringa na Arusha kuanzia Agosti mwaka jana hadi Machi
mwaka huu baada ya kununua tani 2,300 za zao hilo, imeelezwa.
Meneja wa PCT, Martin Oweka alisema hayo
alipoulizwa hatua za kampuni yake kuondoa kero ya wakulima wa zao hilo
waliokuwa wakilalamikia msimu uliopita kutokana na baadhi ya kampuni
kuchukua mazao yao na kuingia mitini.
“PCT Iliwalipa fedha zote baada ya kupima sumu ya
pareto ambayo mwaka huu imeongezeka ubora wake na kusababisha wakulima
wapate fedha nyingi ikilinganishwa na msimu uliopita,” alisema Oweka.
Mkulima wa zao hilo katika Kijiji cha Igale, Mbeya
Vijijini, Admina Mlonzi alisema wakulima waliochuma maua yaliyochanua
na kuyakausha vizuri waliyauza kwa Sh2,400 kwa kilo moja jambo ambalo
linaongeza kasi ya kuboresha uvunaji, ukaushaji na uuzaji ndani ya muda
unaopangwa.
Vijiji vyenye wakulima waliopata fedha nyingi
baada ya kuuza pareto bora ni pamoja na Itale, Igale, Nzoho na Isongole
mkoani Mbeya, wakati upande wa Njombe ni Kitope, Mulondwe na vingine
vipo mikoa ya Manyara na Iringa.
Mkulima Laurent Shila wa Kijiji cha Itale Mbeya
Vijijini, alisema wakulima wa pareto waliofuata maelekezo ya wataalamu
katika uchumaji wa maua, wamepata fedha nyingi na kuna uwezekano wa
miaka ijayo wakulima wengi wakalipenda zao hilo.
Kiwanda cha pareto kilichopo Mufindi, kina uwezo
wa kusindika tani 6,000 kwa mwaka, lakini mwaka huu kimepokea tani
2,300 zilizolimwa na wakulima 25,000 hivyo uongozi wa kiwanda hicho
kudhamiria kuwahamasisha wakulima kulima zao hilo kwa kufuata kanuni
bora ili wanufaike.
0 comments:
Post a Comment